Dar es Salaam. Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imesema kusitishwa kwa huduma ya treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda bara kumesababishwa na kuharibika kwa miundombinu ikiwamo kutitia kwa nguzo mbili kuu katika Daraja la Mto Ruvu, eneo ambalo ukarabati wake kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 1970.
TRL ilisimamisha huduma hizo kuanzia jana baada ya kutokea uharibifu wa miundombinu hiyo jana asubuhi, kati ya Stesheni za Ruvu na makutano ya Ruvu uliosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha maeneo hayo ya Mkoa wa Pwani.
Meneja Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez alisema jana kwamba walijitahidi kuangalia ukubwa wa tatizo lakini mpaka jana mchana walipata taarifa kwamba unahitajika ukarabati mkubwa, hivyo waliamua kusimamisha safari zote kutoka Dar es Salaam.
“Kuna nguzo mbili za Daraja la Mto Ruvu zimetitia, pale kwa kawaida kuna nguzo kama 10 hatuwezi tena kupitisha treni mpaka ufanyike ufundi wa kuinua na kuweka vitu mbadala kwa maana ni nguzo kubwa,” alisema Maez.
Alisema TRL wana utaratibu wa kufanya ukaguzi kila eneo la reli kutambua kasoro zilizopo kabla treni yoyote haijapita.
“Kabla hatujapitisha treni huwa tunafanya uchunguzi na ni kawaida kuna watu wanatembea kilomita 10 kila upande kuangalia reli ilivyo na leo asubuhi ndiyo wakaripoti taarifa hiyo ya hatari. Tumeamua kurudisha fedha za nauli kwa abiria wote waliotakiwa kusafiri,” alisema Maez.
Alipoulizwa reli hiyo itatengamaa lini, Maez alisema kutokana na utaalamu uliofanywa katika eneo hilo na kwa kuzingatia maji yaliyopo, kuna maandalizi maalumu yanafanyika ikiwamo kukusanya vifaa, kutafuta wataalamu na kazi hiyo ya awali ikikamilika ukarabati utaanza haraka.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TRL Mohamed Mapondela, ilieleza kuwa, treni ya kisasa ya abiria (deluxe) iliyokuwa iondoke Dar es Salaam jana saa mbili asubuhi kwenda Kigoma ilifutwa na abiria walitakiwa wafike stesheni ili warejeshewe nauli zao.
Habari zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa tayari uongozi wa TRL umeelekea eneo la tukio ili kufanya tathmini na kupanga mikakati ya haraka kukarabati miundombinu iliyoharibika likiwamo Daraja la Ruvu.
Pia uongozi wa TRL umefafanua katika taarifa yake kuwa katika kipindi cha mpito, treni ya abiria kutoka Kigoma na Mwanza kuja Dar es Salaam itaishia Morogoro hadi njia ya reli kati ya Dar es Salaam na Morogoro itakapofunguliwa tena.
No comments: