Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli jana Sikukuu ya Pasaka, waliungana na Waumini wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni kusali Ibada ya Pasaka.
Katika Ibada hiyo Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba Askofu Charles Salalah aliongoza maombi ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na alimpongeza kwa kazi kubwa ya kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya na kufuja mali za umma.
“Mhe. Rais unafanya kazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua wewe ni majipu madogomadogo yaliyotokana na jipu kuu ambalo ni dhambi za mwanadamu, na jipu hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu, kwa hiyo sisi Wakristo wenzako na waumini wengine tunakuombea sana na tunakuunga mkono katika kazi hii nzito ya kutumbua majipu haya madogomadogo ya watumishi hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na mengine mengi” alisema Askofu Charles Salalah.
Akizungumza katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli aliwashukuru Wakristo wa Kanisa la Africa Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa kuendelea kumuombea na ameomba maombi hayo yaendelee, na pia waiombee nchi iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.
No comments: